Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itachukua miaka 14 kutegua mabomu na kuifanya Gaza kuwa salama tena

Timu ya Umoja wa Mataifa yatathmini uharibifu wa vituo vya matibabu huko Gaza.
© WHO
Timu ya Umoja wa Mataifa yatathmini uharibifu wa vituo vya matibabu huko Gaza.

Itachukua miaka 14 kutegua mabomu na kuifanya Gaza kuwa salama tena

Amani na Usalama

Kuifanya Gaza kuwa tena salama na kutokuwa na mabomu inaweza kuchukua miaka 14 wamesema leo wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa kutegua mabomu.  

Afisa Mkuu wa ofisi ya Umoja Huduma ya uteguzi wa mabomu UNMAS Pehr Lodhammar ameeleza kuwa vita huko Gaza imeacha takriban tani milioni 37 za mabomu na kwamba haiwezekani kubainisha kiasi halisi cha mabomu ambayo bado hayajalipuka katika eneo hilo ambalo hapo awali lilikuwa limejengeka na kuwa na idadi kubwa ya watu lakini sasa limeharibiwa na kubaki vifusi baada ya takriban miezi saba ya mashambulizi makali kutoka Israel. 

Kila mita ya mraba huko Gaza iliyoathiriwa na mzozo huo ina takriban kilo 200 za vifusi, mtaalamu huyo mkongwe wa Umoja wa Mataifa wa kutegua mabomu aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo “Ninachoweza kusema ni kwamba angalau asilimia 10 ya risasi zinazofyatuliwa zinashindwa kufanya kazi ... tunazungumza juu ya miaka 14 ya kazi na lori 100, kwa hivyo hiyo ni miaka 14 itahitajika ili na takriban siku 750,000 za kazi. - siku za kazi za mtu - kuondoa masalia ya mabomu.”

Hamas watakiwa kuwaachilia mateka wote 

Wwakati hayo yakiendelea nchi 18 ikiwemo Marekani wametoa wito hapo jana alhamisi kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia wanashikiliwa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas waliochukuliwa walipovamia eneo la Kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,250.

Israel imesema inaamini kuna mateka zaidi ya 130 bado wanashikiliwa na Hamas huko Gaza kufuatia mashambulizi Oktoba 7, 2023 ambayo yamesababisha Israel kuanza kulishambulia eneo la Gaza na kuua zaidi ya Wapalestina 34,350 na kujeruhi zaidi ya 77,360 kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza. 

Tishio la njaa

Wakati huo huo mashirika ya misaada ya kibinadamu yamerejea onyo lao kwamba njaa inakaribia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, katika ombi jipya la dharura la misaada zaidi kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Israel iliahidi wiki tatu zilizopita kuboresha upatikanaji wa misaada kupitia Kivuko cha Erez kaskazini mwa Gaza na bandari ya mizigo ya Ashdod, kuelekea kaskazini zaidi. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema kumekuwa na ongezeko dogo la misaada lakini si kwa kiasi cha kutosha – au chakuleta  utofauti.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Carl Skau ameeleza kuwa “Bado tunaelekea kwenye baa la njaa, hatujaona mabadiliko ya kimtazamo ambayo yanahitajika kuepusha njaa, tunahitaji kiasi kukubwa zaidi, uingizaji wa misaada unaotabirika zaidi na juhudi endelevu ili kupata usaidizi wa aina mbalimbali kaskazini mwa Gaza.”

Huku kukiwa na ripoti za Israel kutekelez mashambulio huko mashariki mwa Rafah, Bw. Skau alisisitiza wasiwasi kuwa uvamizi wowote wa ardhini katika mji wa kusini wa eneo hilo unahatarisha na kuvuruga ugavi wa misaada ambao tayari hautoshi.

Na tukigeukia juhudi za kuanzisha njia mpya ya kuingiza misaada ya kibinadamu kwa njia ya baharí, afisa huyo wa WFP alisisitiza kuwa "hakuna mbadala wa ardhi" katika kufikisha misaada katika eneo la Gaza.

Israel ruhusu boti zenye misaada kuingia Gaza kwa usalama

Katika tukio linalohusiana na hilo, wataalam wa ngazi ya juu wa haki za binadamu wametoa wito kwa Israel kuhakikisha wanaruhusu boti zilizobeba Msaada wa kibinadamu zinapita salama kuelekea Gaza.

"Flotilla ya Uhuru" inapanga kuondoka nchini Uturuki (Türkiye) ikiwa imebeba tani 5,500 za msaada, pamoja na mamia ya waangalizi wa kimataifa wa kibinadamu, wakielekea Ukanda wa Gaza.

"Wakati Flotilla ya Uhuru inakaribia katika mpaka wa maji wa Wapalestina karibu na Gaza, Israeli lazima ifuate sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na maagizo ya hivi karibuni yaliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhakikisha upatikanaji usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu," walisema wataalam, ambao ni pamoja na Michael Fakhri, Mtaalamu maalum wa masuala ya haki ya chakula.

Mnamo mwaka 2010, wataalamu hao walibaini kuwa Israel ilikamata na kushambulia meli za kiraia za Freedom Flotilla katika eneo la maji la kimataifa, na kuua abiria 10 na kujeruhi wengine wengi.

Wakati huo, Flotilla ya Uhuru ilijaribu kuvunja kizuizi cha Israeli kwa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza.