Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kuikwamua Gaza zikiendelea hatuwezi kuwaambia raia wenye uhitaji wasubiri - UN

Sigrid Kaag, ambaye ni Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza akitembelea jengo la Hospitali ya Nasser huko Khan Younis, Gaza.
OCHA / Olga Cherevko
Sigrid Kaag, ambaye ni Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza akitembelea jengo la Hospitali ya Nasser huko Khan Younis, Gaza.

Harakati za kuikwamua Gaza zikiendelea hatuwezi kuwaambia raia wenye uhitaji wasubiri - UN

Msaada wa Kibinadamu

Jumuiya ya kimataifa ina jukumu na wajibu wa kufanya kazi kufanikisha kukwamuka kwa Gaza lakini hatuwezi kuwaambia raia wasubiri, amesema afisa wa  Umoja wa Mataifa anayehusika na ufikishaji wa misaada kwenye eneo hilo lililozingirwa na Israel.

Sigrid Kaag, ambaye ni Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza, amesema machungu makubwa yanayosababishwa na miezi ya mashambulizi ya makombora nayo pia lazima  yapatiwe ufumbuzi.

“Nadhani ni vigumu sana kwetu sisi na kwenye usalama wa dunia, hata kuanza kuelewa kile ambacho watu wanapitia,” amesema Bi. Kaag akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Ni takribani miezi saba sasa tangu Israel ianzishe mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Gaza kuijbu mashambulizi yaliyoanzishwa na Hamas kwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 na wengine 250 kutekwa nyara.

Zaidi ya wapalestina 34,000 wameuawa Gaza na zaidi ya 77,000 wamejeruhiwa, imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR, ikinukuu mamlaka za afya za Gaza. Hadi leo hii pia watumishi 180 wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA nao pia wameuawa.

Bi. Kaag alikuwa jijini New York, Marekani kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kupitia azimio namba 2720 lilianzisha wadhifa wake huo  mwaka jana, likitoa wito wa Bi. Kaag kufanikisha, kuratibu, kufuatilia na kuthibitisha shehena za misaada zinazongia Gaza.

Akihutubia Baraza hilo leo Alhamisi, Bi. Kaag ametangaza mfumo mpya wa kuingiza Gaza misaada ya kuokoa maisha, mfumo ambao utaanza siku chache zijazo, ikiwa ni moja ya vipengele vya azimio la Baraza la Usalama.

Alizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu kile ambacho kimefanyika hadi sasa na ziara yake ya hivi karibuni huko Gaza, ziara ambayo ni ya nne tangu ateuliwe mwezi Desemba mwaka jana.

Sigrid Kaag: Lengo la ziara yangu ilikuwa kukutana na kuzungumza na kuwa na taarifa kadri iwezekanavyo kuhusu changamoto zilizoko na tunaweza vipi kusonga mbele. Hii ni katika kusaidia watoa misaada ya kiutu wanaofanya kazi kutwa kucha huko Gaza.

Kile nilichoona maeneo mbalimbali ya Gaza ambako tulipita kwa gari, ni kiwango kikubwa cha uharibifu, tulizungumza na watu na kusikia ni kwa vipi wameathirika, vitu walivyopoteza na kiwewe wanachopitia. Na bila shaka, ni kwa vipi wameweza kuhimili katika mazingira haya yasiyo ya kiutu kabisa.

Ziara ya hivi karibuni zaidi ilikuwa kumulika mazingira ya kiafya Gaza, na niliambatana na timu ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO. Tulitembelea kituo cha tiba ya Nasser ambacho kimeharibiwa kabisa. Lakini Mkurugenzi wa Tiba alikuwa tayari amepanga jinsi ya kufanikisha kituo hicho kuanza tena kutoa huduma angalau katika mazingira ya kawaida. Nilitembelea pia kituo cha afya cha IMC ambako kulikuweko na wagonjwa wenye majeruhi makubwa na watoto wenye utapiamlo.

Kwa hiyo basi kwa kuzungumza na wagonjwa na madaktari, na kuguswa na wajibu wa pamoja wa kupunguza machungu na kujaribu kufanya kazi kwa kadri inavyowezekana kufikisha misaada kwa wahitaji kwa njia sio tu endelevu, lakini pia kuwa na mtazamo mpana zaidi ya hali ya sasa.

Idhaa ya UN: Azimio la Umoja wa Mataifa 2720 lililoanzisha wadhifa wako, lilitaka pia kuanzishwa kwa mfumo mpya wa kuongeza kiwango cha misaada ya kiutu inayoingia Gaza. Mmefikia wapi?

Sigrid Kaag: Azimio ni muhimu kwa maeneo makuu mawili: Kufanikisha, kuchagiza na kuharakisha misaada ya kiutu inayoingia Gaza, na pili ni kuanzisha mfumo wa kusaidia hayo yote na hatimaye pia kusaidia juhudi za pamoja za UN na mashirika ya kiraia ya kimataifa na vile vile ya kipalestina na kwa ujumla yamii ya kimataifa. Miezi iliyopita, tumeanzisha kanzidata ya pamoja iliyo jumuishi. Tumeshauriana kuhusu njia za kupita, kile kiitwacho Njia ya Jordan.

Tumekuwa tukishirikiana na wengine kuhusu njia za baharini lakini vile vile kuangalia umuhimu wa njia ya Misri kupitia Rafahili kuhakikisha tuna njia za kutumia kupita, na hatimaye kuongeza kiwango cha shehena na tuweze kufuatilia na kupeana taarifa kufahamu nini kinaingia Gaza kuunga mkono vipaumbele vilivyowekwa na Timu ya Kiutu Gaza. Na kisha ndani ya Gaza, kuelewa kuwa misaada inafikia walengwa na inasambazwa kwa njia bora.

Mfumo sio chombo kitakatifu. Ni jukwaa ambalo linatupatia taswira, unasaidia kuweka vipaumbele na kutupatia takwimu, na hatimaye tuwe na mchakato unaofanyika vizuri. Hivyo tunaondoa mazingira yote ya ucheleweshaji yasiyo ya lazima, tunafahamu kinachoendelea na hatimaye kutupatia uwazi ambao unahitajika.

Sikiliza mahojiano yote hapa kwa lugha ya kiingereza.