Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa kuchukua hatua kuepusha baa la njaa Sudan ni sasa - Rein Paulsen

Rein Paulsen, Mkurugenzi wa Ofisi ya Dharura na Ustahimilivu ya FAO, akikutana na mkulima huko Tobin, Sudan tarehe 17 Aprili, 2024.
© FAO / Mahmoud Shamrouk
Rein Paulsen, Mkurugenzi wa Ofisi ya Dharura na Ustahimilivu ya FAO, akikutana na mkulima huko Tobin, Sudan tarehe 17 Aprili, 2024.

Wakati wa kuchukua hatua kuepusha baa la njaa Sudan ni sasa - Rein Paulsen

Msaada wa Kibinadamu

Katika mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, afisa mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) anayehusika na masuala ya dharura na mnepo, Rein Paulsen ametahadharisha kuwa hatari ya kutokea baa la njaa nchini Sudan ni halisi na kwa hivyo wakati wa kuchukua hatua ni sasa. 

Akizungumza kutoka katika mji wa Port of Sudan nchini Sudan mwishoni mwa wiki, Rein Paulsen anasema, "tuna mkakati katika maeneo matatu. Kipengele muhimu ni katika mazao kwa misimu miwili mikuu. Kwa hivyo nafaka kwa msimu huu ujao na mbogamboga muhimu kwa msimu wa pili, lakini pia kuzingatia mifugo.”

Anaongeza kwamba, “hivyo kuweza kusaidia mifugo hiyo kwa lishe ya dharura, kwa chanjo muhimu, ambazo zote zinasaidia kuhakikisha kaya ambazo hazina chakula zinaendelea, kwa mfano, kupata maziwa kutoka kwa mbuzi wao. Yote haya ni muhimu katika juhudi za kuzuia njaa."

Kuhusu ufadhili, Rein Paulsen anafafanua kuwa, "FAO kwa sasa inahitaji dola milioni 104 kusaidia zaidi ya Wasudan milioni 10 Sudan mwaka huu wa 2024. Tunafadhiliwa chini ya asilimia 10. Kwa hivyo, suala la ufadhili ni changamoto ya kweli. Mara nyingi tunazungumza kuhusu hili, lakini tuna ufadhili mdogo mwaka huu kuliko tulivyofanya mwaka jana. Na hali ya uhaba wa chakula ni mbaya zaidi mwaka huu kuliko mwaka jana. Kwa hivyo mielekeo hiyo miwili, ilibidi ipate mwelekeo mbaya."

Mkurugenzi wa OER Rein Paulsen akikutana na viongozi wa eneo hilo na wakulima katika kijiji cha Shata, Sudan - 17 Aprili 2024.
© FAO / Mahmoud Shamrouk
Mkurugenzi wa OER Rein Paulsen akikutana na viongozi wa eneo hilo na wakulima katika kijiji cha Shata, Sudan - 17 Aprili 2024.

Anashauri akisema, “Tunahitaji kuongozwa na ushahidi. Tunahitaji kuzingatia mazingira na hali hizo ambapo tuna viwango vya juu vya uhaba wa chakula, na kuna haja ya kuwa na ufadhili unaolingana na kiwango cha mahitaji yaliyopo. Na sisi, tunahisi sana kuwa Sudan inafaa na inastahili kuangaliwa zaidi kuliko inavyopokea kwa sasa.”

Kuhusu upatikanaji wa ardhi, afisa huyo mwandamizi wa FAO anasema pia wanaguswa kusikia ripoti kutoka kwa wakulima kuhusu kutokuwa na uwezo wa kupata mashamba.

"Na kwa hivyo, unajua, kwetu kama shirika maalumu la kiufundi, sio tu kuhusu kutoa pembejeo kwa wakulima. Pia tunatoa usaidizi wa kiufundi, lakini ni wazi wanahitaji ufikiaji wa ardhi yao ili kuitayarisha. Wanahitaji kupata ardhi ya kupanda. Wanahitaji kupata ardhi, kufuatilia na kuangalia mazao yao na kisha kupata ardhi ili waweze kuvuna kwa wale wanaopanda mazao. Na kwa hivyo, suala hili la, kuweza kupata ardhi ya kilimo ni muhimu na kipaumbele kikuu na wasiwasi."

Anahitimisha akisema, "Nifupishe tu kwamba ushahidi unaonesha kuwa hatari ya baa la njaa iko hapa, tuna fursa ya kuizuia. Dirisha hilo la fursa linapokuja suala la msaada wa dharura wa kilimo ni sasa. Msimu mkuu wa kupanda huanza katika wiki chache tu, lakini inawezekana kufanya kazi katika mwaka mzima wa kalenda ili kukabiliana na hali hiyo. Tunahitaji mwitikio wa sekta mbalimbali ili kuwa na mpango madhubuti wa kuzuia njaa. Na kwa hivyo, ni wazi kwa Shirika la Chakula na Kilimo, ninazungumza juu ya kazi ya dharura ya kilimo ambayo inapaswa kufanyika, lakini ni muhimu vile vile kwa vyombo maalum vinavyofanya kazi, masuala ya afya, masuala ya lishe, kuhusu maji, kwamba wote hao wapate usaidizi kwa mkakati madhubuti wa kuzuia baa la njaa kutokea. Tunajua tunaweza kufanya hivyo kwa kiwango kikubwa. Tumewahi kufanya hivyo katika siku za nyuma, lakini tunahitaji usaidizi ili kuweza kufanya hivyo tunapoelekea katika miezi ijayo.”